Ijumaa, 15 Mei 2015

KAMUSI YA LUGHA; MAANA, AINA, TAARIFA NA DHIMA ZAKE.



KAMUSI YA LUGHA; MAANA, AINA, TAARIFA NA DHIMA ZAKE.

MAANA YA KAMUSI
Massamba (2012:24) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno katika lugha, yaliyopangwa kwa utaratibu maalum, pamoja na maana au fasili zake; katika uchanganuzi wa lugha haya ni maneno ya kileksika, yaani yasiyokuwa ya kisarufi au kifonolija.
Tuki (1990:21) kamusi ni kitabu cha orodha ya maneno yaliyopangwa kwa utaratibu maalum, pamoja na maana na fasili zake.
Wamitila (2003:76) kamusi ni kitabu ambacho kina orodha ya maneno katika lugha Fulani ana ambayo hupangwa ki-abjadi au kialfabeti. Maneno haya huelezewa maana zake mbalimbali na labda hata vyanzo vyake.
Matinde (2012:273) kamusi ni kitabu chenye mkusanyiko wa maneno sanifu katika lugha mahususi yaliyoorodheshwa kialfabeti na kutoa taarifa za kifonetiki, kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, na hata kisemantiki.
Nyambari na Masebo (2012:179) kamusi ni kitabu cha marejeleo chenye msamiati uliokusanywa kutoka kwa wazungumzaji wa jamii fulani, na kupangwa kwa utaratibu maalumu, kisha kufafanuliwa kwa namna ambayo msomsji huweza kuelewa.
Kwa ujumla  kamusi ni kitabu chenye orodha ya maneno mbalimbali yaliyopangwa vizuri kwa kufuata alfabeti na hutoa taarifa mbalimbali kama vile maana, matamshi n.k.

MUUNDO WA KAMUSI
i)  Utangulizi wa Kamusi
Hii ni sehemu ya mwanzo ambayo hutangulia matini yenyewe ya kamusi.
ii)  Matini ya Kamusi
Hii ni sehemu ambayo inaonyesha vidahizo na fahiwa zake kuanzia herufi A-Z.
iii)  Sherehe ya Kamusi
hizi ni baadhi ya taarifa ambazo huwa zimeandikwa mwishoni mwa kamusi. Kwa mfano majina ya nchi, lugha za mataifa duniani, vipimo vya urefu, vipimo vya uzito, ujazo  n.k.

AINA ZA KAMUSI
Kwa kutumia kigezo cha LUGHA kuna aina kuu tatu (3) za kamusi
i) kamusi wahidiya
hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha moja
ii) kamusi thaniya
Hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha mbili.
iii) kamusi mahuluti
Hii ni kamusi inayoandikwa kwa lugha zaidi ya mbili. Kwa mfano Kiswahili-kiingereza-kifaransa.

Taaarifa zinazopatikana katika kamusi
Taarifa hizi huweza kuwa za kisarufi au kileksika
a) taarifa za kisarufi zinazoingizwa katika kamusi.
Nyambari na Masebo (2012:184) wameainisha taarifa zifutazo za kisarufi zinazopatikana katika kamusi.
·       Wingi wa nomino
·       Kategoria ya kisarufi ya kidahizo mf. Kitenzi (kt), nomino (nm) n.k
·       Vinyumbuo vya vitenzi mf. Piga-pigwa-pigana-pigika n.k
·       Ngeli za nomino mf. Mtu (A-YU), kazi (i-)
·       Matamshi ya neno
·       Elekezi au sielekezi. Mfano: Apiza kt  [ele], Anguka kt  [sie]
·       Mifano ya matumizi

b) Taarifa za kileksia zinazopatikana katika kamusi
Matinde (2012:275-281) anaeleza taarifa zifuatazo za kileksia ambazo zinapatikana katika kamusi ya lugha.
·       Mpangilio wa vidahizo
·       Kategoria za maneno
·       Umoja na wingi
·       Upatanisho wa kisarufi
·       Uelekezi wa vitenzi
·       Maana ya vidahizo
·       Tahajia za maneno
·       Mifano ya matumizi
·       Methali, nahau na misemo
·       Timolojia ya leksimu
·       Michoro/ picha
·       Matamshi
DHIMA ZA KAMUSI
·       Huonesha tahajia sahihi za maneno
·       Huonesha maana za maneno
·       Huonesha matamshi sahihi ya maneno
·       Huonesha asili ya neno
·       Humsaidia mtumiaji kujifunza lugha za kigeni
·       Huonesha alama na vifupisho mbalimbali katika lugha husika.


                     Marejeleo
Massamba. D.P.B.(2004 ). Kamusi ya isimu na falsafa ya lugha. Dares salaam: TUKI
Masebo . J. A. & Nyangwine. N. (2012). Kiswahili kidato cha tatu na nne . Dares salaam: nyambari nyangwine publishers
Matinde. R. S. (2012). Dafina ya lugha. Isimu na nadharia. Kwa sekondari, vyuo va kati na vyuo vikuu. Mwanza : Serengeti bookshop.
TUKI (1990).kamusi sanifu ya isimu na lugha. Dares salaam: Tuki na Educational publishers and distributors ltd.
Wamitila. K. W. (2003). Kamusi ya fasihi, istilahi na nadharia. Nairobi: Focus publishers ltd.




Jumatatu, 20 Aprili 2015

FASIHI SIMULIZI; MAANA, SIFA NA TANZU ZAKE.



FASIHI SIMULIZI; MAANA, SIFA NA TANZU ZAKE.

Maana ya fasihi simulizi
 Balisidya (1983) Fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo hutumia mdomo katika kuumbwa, kuwasilishwana kusambazwa kwa wasikilizaji na watumiaji wake.
 Msokile, M (1992) anasema kuwa fasihi simulizi ni kazi ya sanaa inayotumia lugha ya mazungumzo ya ana kwa ana, sauti na vitendo na njia zote za mawasiliano kufikisha ujumbe kwa jamii.
 Mulokozi , M. M (1996) anasema kuwa fasihi simulizi ni fasihi inayotungwa au kubuniwa kichwani na kuwasilishwa kwa hadhira kwa njia ya mdomo na vitendo bila kutumia maandishi.

Sifa za fasihi simulizi
1. huwasilishwa kwa matamshi kupitia mdomo
2. ni kongwe
3. uwasilishaji wake ufungamana na vitendo
4. ni mali ya jamii na wala haimilikiwi na mtu maalumu
5. huwa na hadhira tendi (hadhira hushirikishwa)
6. hubadilika kutokana na muktadha na fanani husika
7. huwa na wakati na muktadha maalumu
8. huifadhiwa akilini mwa wanajamii husika na utendaji wake hutegemea uwezo wao wa kukumbuka

Tanzu za fasihi simulizi
Kuna tanzu kuu nne za fasihi simulizi ambazo ni semi, ushairi, maigizo na hadithi LAKINI kila tanzu ina vijitanzu vidogo vidogo kama ifuatavyo:

1. semi
·       Methali
·       Vitendawili
·       Misimu
·       Mafumbo
·       Lakabu
   
2. ushairi
·       Nyimbo
·       Ngonjera
·       Mashairi
·       Maghani

3. maigizo
·       Ngomezi
·       Vichekesho
·       Ngonjera
·       Majigambo
·       Mazungumzo
·       Malumbano ya utani
·       Mivigha
·       Ulumbi

4. hadithi
·       Hekaya
·       Visasili
·       Visakale
·       Ngano
·       Vigano
·       Soga
·       Tarihi

MAREJELEO
Tuki(2004).Kamusi ya Kiswahili Sanifu..Nairobi:  Oxford University Press East Africa Ltd

Mulokozi, M.M (1996),Utangulizi wa Fasihi Simulizi ya Kiswahili. Dares Salaam: Oxford Univeristy 
Press.      
    
Senkoro,F.E.M.K(2011) Fasihi. Dares Salaam:  KAUTTU Limited.

Msokile, M. (1992).Kunga za fasihi na lugha. Dares Salaam:  Educational Publishers and Distributors.
Wanjala, F, S, (2011), Kitovu Cha Fasihi Simulizi: Kwa Shule, Vyuo Na Ndaki, Mwanza: Serengeti bookshop.

Jumatano, 1 Aprili 2015

MAANA NA MIFANO YA VISAWE, VINYUME, VITAWE, NA UMERONIMIA KWA KUTUMIA LUGHA ZA KIBANTU.

MAANA NA MIFANO YA VISAWE,  VINYUME,  VITAWE, NA UMERONIMIA KWA KUTUMIA

 LUGHA ZA KIBANTU.


Visawe
Kwamujibu wa matinde (2012:267) visawe ni maneno yenye maana zinazokaribiana. Kwa mfano  “uchawi” na “urogi” humaanisha kitu kimoja.     Vilevile tunaweza kusema kuwa visawe ni maneno tofauti yenye maana sawa. Ifuatayo ni mifano ya visawe kutoka katika lugha mbalimbali za kibantu:
Kingindo
Katika lugha ya kingindo kuna Maneno mengi ambayo husimama kama visawe, kwa mfano maneno Anamuungu na Nnongo yote haya humaanisha neno moja tu ambalo ni “Mungukatika lugha ya kiswahili.
Kimatumbi
Mfano wa visawe katika lugha hii ni kama vile “Anamuungu” naMnungu” yote haya humaanisha neno moja tu ambalo ni Mungu” katika lugha ya Kiswahili.
Kinyaturu
Katika lugha hii ya kinyaturu pia kuna maneno mbalimbali ambayo huwa na maana sawa ijapokuwa yanatamkwa na kuandikwa tofauti, kwa mfano maneno kama vile Idimu” na Inkhuu” haya yote humaanisha Nyumba” katika lugha ya Kiswahili.
   Vinyume
Kwa mujibu wa matinde (2012:264) anaeleza kuwa vinyume ni uhusiano wa kimuundo ambapo fahiwa ya maneno hupingana. Aidha, ni neno ambalo maana yake huwa ni kinyume cha neno linguine. Kuna aina mbalimbali za vinyume zikiwemo vinyume vya utoano, vinyume vya vidato, vinyume vya tofauti mkabala, vinyume vya uelekeo, vinyume vya tathmini, na vinyume vya utenduzi. Mfano wa vinyume katika lugha ya Kiswahili ni kama vile kufa-kuishi, dada-kaka, kaskazini-kusini, nenda-rudi, funga-fungua n.k. Ifuatayo ni mifano ya vinyume katika lugha mbalimbali za kibantu.

Kingindo
Kama ilivyo katika lugha nyingine za kibantu lugha ya kingindo pia ina maneno mbalimbali ambayo ni vinyume, mfano mzuri wa maneno hayo ni Akata-Atendaliengo yakimaanisha Mvivu-Mchapakazi katika Kiswahili, pia maneno kama vile Aganja-Abya ambayo humaanisha Rafiki-Adui katika lugha ya Kiswahili.
Kimatumbi
Maneno ambayo husimama kama vinyume katika lugha ya kimatumbi ni kama vile Mkataa-Mpangakachi ambayo humaanisha Mvivu-Mchapakazi katika lugha ya Kiswahili, pia maneno kama vile mbwiga-abya humaanisha Rafiki-Adui katika lugha ya Kiswahili.
Kihehe
Katika lugha ya kihehe kuna maneno mengi sana ambao ni vinyume, maneno yafuatayo yanabainisha dhahiri dhana hii na vinyume: Kukita-Kuwuka ambayo humaanisha Kwenda-Kurudi katika lugha yetu ya Kiswahili, pia maneno kama vile Mhinza-Mkwamidzi ambayo humaanisha Msichana-Mvulana katika lugha ya Kiswahili husimama kama vinyume.
                          Kutokana na mifano iliyobainishwa hapo juu tunabaini kuwa tofauti kuu kati ya visawe na vinyume ni kwamba visawe ni maneno tofauti tofauti ambayo huwa na maana sawa ilihali vinyume ni maneno ambayo hutamkwa na kuandikwa tofauti na hutoa maana zinazokinzana.

   Umeronimia
Kwa mujibu wa matinde (2012:267) meronimia ni dhana inayotumiwa kuelekeza uhusiano wa kitu kizima na sehemu zake au vijenzi vyake. Kwa mfano neno Mwili- amabalo hujuisha kichwa, masikio, tumbo, miguu, mikono, pua n.k. ifuatayo ni mifano ya maneno kutoka lugha za kibantu ambayo hubainisha dhana hii ya umeronimia:

Kichaga
Lugha ya kichaga ina maneno mengi ambayo hubainisha dhana hii ya umeronimia, maneno hayo ni kama vila, IKIRI- mambagha, nyikiri, mri, marha ambapo kwa Kiswahili humaanaisha MTI- matawi, shina, mzizi, majani. Pia kuna maneno mengine kama vile MNDIU- marende, maoko, mro, ndeu ambayo humaanisha MWILI- miguu, mikono, kichwa, tumbo katika lugha ya Kiswahili.
Kinyakyusa
Kwa upande wa lugha ya kinyakusa pia haipo nyuma kwani kuna maneno mbalimbali ambayo huweza kusimama kama umeronimia. Mfano mzuri wa maneno ya kinyakusa ambayo husimama kama umeronimia ni kama vile INJENGE- lwighi, iluto ambayo kwa upande wa Kiswahili humaanisha NYUMBA- mlango, dirisha.
Kinyaturu
Kinyaturu kama ilivyo katika lugha nyingine kama vile kichaga na kinyakyusa pia lugha hii ina maneno ambayo yanabainisha moja kwa moja dhana hii ya umeronimia. Kuna mifano mingi sana ambayo inabainisha dhana hii ya umeronimia, mfano mzuri wa maneno hayo ni kama vile: MWIRII- mnkono, mnghuu, itywe, ndaa ambayo humaanisha MWILI- mkono, mguu, kichwa, tumbo katika lugha ya Kiswahili. Pia kuna maneno mengine kama vile MNTYII- mirii, mantambi, intyina ambayo humaanisha MTI- mizizi, matawi, shina katika lugha ya kiswahili.
 Vitawe
Kwa mujibu wa matinde (2012:262) vitawe ni muundo wenye maneno mbalimbali ambayo yanahusiana kimaana na mara nyingi ya maneno hayo huwa imepanuka kadri ya mpito wa wakati. Vitawe mara nyingi huwa na uhusiano kihistoria. Vilevile vitawe huweza kufasiriwa kama ni maneno yenye maana zaidi ya moja. Kwa mfano neno paa ambalo humaanisha enda juu, mnyama, na sehemu ya juu ya nyumba. Zifuatazo ni lugha za kaibantu na mifano yake juu ya dhana hii ya vitawe:


Kichaga
Katika lugha ya kichaga maneno yafuatayo yanabainisha dhana hii ya vitawe: neno “Mangi” ambalo humaanisha “mungu” pamoja na “mwanamume”
Kinyakusa
Kwa upande wa lugha ya kinyakyusa kuna maneno mbalimbali ambayo yanabainisha wazi dhana hii ya viawe. Maneno yafuatayo yanabainisha moja kwa moja dhana hii ya visawe: Taka” ambalo humaanisha mungu pamoja na kijana wa kiume, pia neno kama vile “Kisa” ambalo humaanisha huruma, huzuni, na upole, vilevile kuna neno kama vile Hobhokela” ambalo humaanisha samehe, huruma na achilia katika lugha ya Kiswahili.
                     Kutokana na ufafanuzi uliotolewa hapo juu tunabaini kuwa tofauti iliyopo baina ya uremonimia na vitawe ni kwamba uremonimia ni neno la jumla linaloonesha mjumuiko wa vitu vilivyokiunda kitu hicho wakati vitawe ni maneno yanayowakilisha maana zaidi ya moja.


                                             MAREJELEO
Matinde, R, S. (2012). Dafina ya Lugha Isimu na Nadharia. Kwa Sekondari, Vyuo vya kati na  Vyuo vikuu. Serenget Bookshop: Mwanza.
Wikipedia the free encyclopedia/ visawe/ vinyume.